LSF YAFANYA TATHMINI UTEKELEZAJI PROGRAMU YA
UPATIKANAJI HAKI MWAKA NCHINI 2021
Jumatano Oktoba 20, 2021: Dodoma
Shirika la Legal Services Facility (LSF) ambalo linajishughulisha
na kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa raia wote nchini hususani wanawake
kupitia uwezeshaji wa kisheria linaendesha mkutano wa siku mbili kwa mashirika
wanufaika wake pamoja na wadau wake kutoka Tanzania bara na Zanzibar, Jijini
Dodoma kuanzia leo 20 Oktoba 2021 mpaka kesho 21 Oktoba 2021.
Mkutano huu wa siku mbili unajumuisha washiriki takribani 200
ikiwemo Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Watoa huduma za msaada wa kisheria na
wasaidizi wa kisheria kutoka mikoa yote nchini Tanzania. Vilevile mkutano
huu unajumuisha mashirika wanufaika wa mradi wa uwezeshaji kisheria katika
maeneo ya mijini (Urban Legal Empowerment Grantees) pamoja na wadau wengine
muhimu kutoka katika sekta ya msaada wa kisheria nchini Tanzania.
Mkutano huo unalenga hasa kutoa wigo wa kubadilishana taarifa
kuhusu matokeo ya programu na kujadili pamoja kwa umuhimu na kimkakati
mafanikio ya LSF kwa miaka ijayo zaidi baada ya mwaka 2021 kwa wanufaika na
wadau wote wa LSF. Hii inakuja kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa
LSF wa miaka mitano ijayo unaotarajia kuanza mwakani 2022 mpaka 2026.
Mkutano huu unalenga kukuza ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa
huduma, ushirikishaji wa wananchi katika mifumo ya huduma za msaada wa kisheria
kwa ajili ya kuchochea ukuaji na ustawi wa uwajibikaji, ushiriki na
ujumuishwaji wa raia katika mifumo ya uwezeshaji wa kisheria nchini.
Kikubwa zaidi, katika mkutano huo, LSF pamoja na wadau wake
wanalenga kujionea bayana pamoja na kujifunza kuhusu hali ya maendeleo na
matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na wanufaika wa LSF
katika kipindi hiki cha mpito 2021 baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa awamu
ya pili ya program miaka mitano (2016 -2020) hapo Disemba 2020.
Vilevile, mkutano huo unalenga kutambua jitihada na juhudi za
Wasaidizi wa Kisheria nchini waliowezeshwa moja kwa moja na LSF pamoja na
kujadili malengo ya baadaye kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa
2022-2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu Mkurugenzi wa Idara
ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na
Utawala Bora Visiwani Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said amesema kuwa mkutano huo
ni muhimu kwakuwa unawaleta pamoja wadau msaada wa kisheria ambao wamekuwa ni sehemu
kubwa ya mafanikio katika kukuza upatikanaji wa haki nchini.
“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta ya msaada wa
kisheria. Kumekuwa na taabu mbalimbali katika jamii ambazo husababishwa
na ukandamizaji wa haki mbalimbali ikiwemo wanawake na Watoto. Kupitia programu
ya LSF na wadau wake nchini mmeweza kufanya kazi kubwa ya kusaidia jamii
kupitia uwezeshaji wa kisheria.” Amesema Hanifa.
Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe
amesema kuwa anaamini kuwa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa program ya
upatikanji wa haki nchini Tanzania litakwenda sambamba na wadau wote wa sekta
ya msaada wa kisheria kuelekezana kuhusu kutii matakwa ya kisheria juu ya
uendeshaji wa taasisi au mashirika yanatoa huduma za msaada wa kisheria na
wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania.
“Kupitia mkutano huu ningependa kuwakumbusha kuendelea kutii
sheria. Najua waliopo katika mkutano huu ni wakurugenzi ambao ndio
watendaji wakuu wa taasisi zenu. Niwaombe kutii sheria zote kama
inavyotakiwa. Kuzingatia sheria zilizowekwa inarahisisha utendaji wenu
kwakuwa inasaidia taasisi zenu kutambulika na mamlaka mbalimbali za
kiserikali,” amesema Wakili Mkawe.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa
amefurahi kukutana na wadau wake wote ambao amekuwa akifanya nao kazi nchi
nzima, ambapo kwa kipindi cha miaka kumi wameweza kupata mafanikio mbalimbali
ikiwemo kuundwa kwa sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017.
“Nafurahi kukutana na
wadau wetu wakubwa ambao mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kutekeleza program yetu
ya upatikanaji haki nchi nzima. Naona fahari kuona kuwa LSF sasa
imetimiza miaka 10 tangu ianze kutekeleza program yake na kupitia mashirika
wanufaika wake tumefikia mfanikio mbalimbali ya sekta ya msaada wa
kisheria. Naamini kuwa baada ya kikao hiki kazi yetu itaendelea kwa kasi
zaidi ili kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kupitia huduma bora za msaada wa
kisheria,” amesema Lulu Ng’wanakilala.
MWISHO=======================