Shirika
la Legal Services Facility (LSF) ambalo linajishughulisha na kazi ya kukuza
upatikanaji wa haki kwa raia wote nchini hususani wanawake kupitia uwezeshaji
wa kisheria linaendesha mkutano wa siku mbili kwa mashirika wanufaika wake
pamoja na wadau wake kutoka Tanzania bara na Zanzibar, Jijini Dodoma kuanzia
leo 20 Oktoba 2021 mpaka kesho 21 Oktoba 2021.
Mkutano
huu wa siku mbili unajumuisha washiriki takribani 200 ikiwemo Watendaji Wakuu
wa Mashirika ya Watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria
kutoka mikoa yote nchini Tanzania. Vilevile mkutano huu unajumuisha
mashirika wanufaika wa mradi wa uwezeshaji kisheria katika maeneo ya mijini
(Urban Legal Empowerment Grantees) pamoja na wadau wengine muhimu kutoka katika
sekta ya msaada wa kisheria nchini Tanzania.
Mkutano
huo unalenga hasa kutoa wigo wa kubadilishana taarifa kuhusu matokeo ya
programu na kujadili pamoja kwa umuhimu na kimkakati mafanikio ya LSF kwa miaka
ijayo zaidi baada ya mwaka 2021 kwa wanufaika na wadau wote wa LSF. Hii inakuja
kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa LSF wa miaka mitano ijayo
unaotarajia kuanza mwakani 2022 mpaka 2026.
Mkutano
huu unalenga kukuza ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa huduma, ushirikishaji wa
wananchi katika mifumo ya huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuchochea
ukuaji na ustawi wa uwajibikaji, ushiriki na ujumuishwaji wa raia katika mifumo
ya uwezeshaji wa kisheria nchini.
Kikubwa
zaidi, katika mkutano huo, LSF pamoja na wadau wake wanalenga kujionea bayana
pamoja na kujifunza kuhusu hali ya maendeleo na matokeo ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali inayotekelezwa na wanufaika wa LSF katika kipindi hiki cha
mpito 2021 baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa awamu ya pili ya program
miaka mitano (2016 -2020) hapo Disemba 2020.
Vilevile,
mkutano huo unalenga kutambua jitihada na juhudi za Wasaidizi wa Kisheria
nchini waliowezeshwa moja kwa moja na LSF pamoja na kujadili malengo ya baadaye
kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa 2022-2026.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mkutano huu Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria
kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na Utawala Bora Visiwani
Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwakuwa
unawaleta pamoja wadau msaada wa kisheria ambao wamekuwa ni sehemu kubwa ya
mafanikio katika kukuza upatikanaji wa haki nchini.
“Mkutano
huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta ya msaada wa kisheria. Kumekuwa na
taabu mbalimbali katika jamii ambazo husababishwa na ukandamizaji wa haki
mbalimbali ikiwemo wanawake na Watoto. Kupitia programu ya LSF na wadau wake
nchini mmeweza kufanya kazi kubwa ya kusaidia jamii kupitia uwezeshaji wa
kisheria.” Amesema Hanifa.
Wakili
wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe amesema kuwa
anaamini kuwa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa program ya upatikanji wa haki
nchini Tanzania litakwenda sambamba na wadau wote wa sekta ya msaada wa
kisheria kuelekezana kuhusu kutii matakwa ya kisheria juu ya uendeshaji wa
taasisi au mashirika yanatoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa
kisheria nchini Tanzania.
“Kupitia
mkutano huu ningependa kuwakumbusha kuendelea kutii sheria. Najua waliopo
katika mkutano huu ni wakurugenzi ambao ndio watendaji wakuu wa taasisi zenu.
Niwaombe kutii sheria zote kama inavyotakiwa. Kuzingatia sheria
zilizowekwa inarahisisha utendaji wenu kwakuwa inasaidia taasisi zenu
kutambulika na mamlaka mbalimbali za kiserikali,” amesema Wakili Mkawe.
Nae
Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa amefurahi kukutana
na wadau wake wote ambao amekuwa akifanya nao kazi nchi nzima, ambapo kwa
kipindi cha miaka kumi wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa
sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017.
“Nafurahi kukutana na wadau
wetu wakubwa ambao mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kutekeleza program yetu ya
upatikanaji haki nchi nzima. Naona fahari kuona kuwa LSF sasa imetimiza
miaka 10 tangu ianze kutekeleza program yake na kupitia mashirika wanufaika
wake tumefikia mfanikio mbalimbali ya sekta ya msaada wa kisheria. Naamini
kuwa baada ya kikao hiki kazi yetu itaendelea kwa kasi zaidi ili kuwa na jamii
iliyowezeshwa kisheria kupitia huduma bora za msaada wa kisheria,” amesema Lulu
Ng’wanakilala.
MWISHO