• admin
  • News & Updates
  • No Comments

LSF YAFANYA TATHMINI UTEKELEZAJI PROGRAMU YA UPATIKANAJI HAKI MWAKA NCHINI 2021

Jumatano Oktoba 20, 2021:  Dodoma 

Shirika la Legal Services Facility (LSF) ambalo linajishughulisha na kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa raia wote nchini hususani wanawake kupitia uwezeshaji wa kisheria linaendesha mkutano wa siku mbili kwa mashirika wanufaika wake pamoja na wadau wake kutoka Tanzania bara na Zanzibar, Jijini Dodoma kuanzia leo 20 Oktoba 2021 mpaka kesho 21 Oktoba 2021.

Mkutano huu wa siku mbili unajumuisha washiriki takribani 200 ikiwemo Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria kutoka mikoa yote nchini Tanzania.  Vilevile mkutano huu unajumuisha mashirika wanufaika wa mradi wa uwezeshaji kisheria katika maeneo ya mijini (Urban Legal Empowerment Grantees) pamoja na wadau wengine muhimu kutoka katika sekta ya msaada wa kisheria nchini Tanzania.

Mkutano huo unalenga hasa kutoa wigo wa kubadilishana taarifa kuhusu matokeo ya programu na kujadili pamoja kwa umuhimu na kimkakati mafanikio ya LSF kwa miaka ijayo zaidi baada ya mwaka 2021 kwa wanufaika na wadau wote wa LSF. Hii inakuja kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa LSF wa miaka mitano ijayo unaotarajia kuanza mwakani 2022 mpaka 2026.

Mkutano huu unalenga kukuza ufanisi wa kiutendaji, utoaji wa huduma, ushirikishaji wa wananchi katika mifumo ya huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuchochea ukuaji na ustawi wa uwajibikaji, ushiriki na ujumuishwaji wa raia katika mifumo ya uwezeshaji wa kisheria nchini.

Kikubwa zaidi, katika mkutano huo, LSF pamoja na wadau wake wanalenga kujionea bayana pamoja na kujifunza kuhusu hali ya maendeleo na matokeo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na wanufaika wa LSF katika kipindi hiki cha mpito 2021 baada ya kumalizika kwa utekelezaji wa awamu ya pili ya program miaka mitano (2016 -2020)  hapo Disemba 2020.

Vilevile, mkutano huo unalenga kutambua jitihada na juhudi za Wasaidizi wa Kisheria nchini waliowezeshwa moja kwa moja na LSF pamoja na kujadili malengo ya baadaye kuelekea utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa 2022-2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi, na Utawala Bora Visiwani Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwakuwa unawaleta pamoja wadau msaada wa kisheria ambao wamekuwa ni sehemu kubwa ya mafanikio katika kukuza upatikanaji wa haki nchini.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa sekta ya msaada wa kisheria.  Kumekuwa na taabu mbalimbali katika jamii ambazo husababishwa na ukandamizaji wa haki mbalimbali ikiwemo wanawake na Watoto. Kupitia programu ya LSF na wadau wake nchini mmeweza kufanya kazi kubwa ya kusaidia jamii kupitia uwezeshaji wa kisheria.” Amesema Hanifa.

Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Agness Mkawe amesema kuwa anaamini kuwa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa program ya upatikanji wa haki nchini Tanzania litakwenda sambamba na wadau wote wa sekta ya msaada wa kisheria kuelekezana kuhusu kutii matakwa ya kisheria juu ya uendeshaji wa taasisi au mashirika yanatoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania.

“Kupitia mkutano huu ningependa kuwakumbusha kuendelea kutii sheria.  Najua waliopo katika mkutano huu ni wakurugenzi ambao ndio watendaji wakuu wa taasisi zenu. Niwaombe kutii sheria zote kama inavyotakiwa.  Kuzingatia sheria zilizowekwa inarahisisha utendaji wenu kwakuwa inasaidia taasisi zenu kutambulika na mamlaka mbalimbali za kiserikali,” amesema Wakili Mkawe.

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa amefurahi kukutana na wadau wake wote ambao amekuwa akifanya nao kazi nchi nzima, ambapo kwa kipindi cha miaka kumi wameweza kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuundwa kwa sheria ya msaada wa kisheria mwaka 2017.

“Nafurahi kukutana na wadau wetu wakubwa ambao mmekuwa mkifanya kazi kubwa ya kutekeleza program yetu ya upatikanaji haki nchi nzima.  Naona fahari kuona kuwa LSF sasa imetimiza miaka 10 tangu ianze kutekeleza program yake na kupitia mashirika wanufaika wake tumefikia mfanikio mbalimbali ya sekta ya msaada wa kisheria.  Naamini kuwa baada ya kikao hiki kazi yetu itaendelea kwa kasi zaidi ili kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kupitia huduma bora za msaada wa kisheria,” amesema Lulu Ng’wanakilala.

MWISHO=======================

 

Kwa Muhtasari:

Legal Services Facility (LSF) ni mfuko wa fedha ulioanzishwa mwaka 2011 kama shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki kwa wote, hasa wanawake kwa njia ya uwezeshaji wa kisheria.  LSF hutoa fedha kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa mawasiliano zaidi tembelea tovuti yetu www.lsftz.org au wasiliana na;

Jane Matinde- Meneja wa Mawasiliano, LSF

Barua pepel:  jane.matinde@lsftz.org

Simu:  +255784 670 232

AU

Mtapa Kitwaza- Afisa Mawasiliano, LSF

Barua pepe:  mtapa.kitwaza@lsftz.org

Simu:  +255684 738 499

 

Author: admin

Leave a Reply

7 + 20 =