• admin
  • News & Updates
  • No Comments

RASIMU YA HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA MAADHIMISHO YA MIAKA KUMI YA TAASISI YA LEGAL SERVICES FACILITY (LSF)

DAR ES SALAAM: TAREHE 11 NOVEMBA 2021

Mh. Geofrey Pinda (MB), Naibu Waziri wa Sheria na Katiba;

Mh. Doroth Gwajima(MB) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto;

Wawakilishi kutoka Wizara na Idara mbalimbali za serikali kutoka Serikali ya jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mliopo hapa;

Dr. John Jingu  Katibu Mkuu wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto;

Katibu Mkuu Ofisi ya  Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Seif Shaaban Mwinyi;

Ndg. Beng’i Issa Mazana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- Taasisi ya Legal Services Facility(LSF);

Ndg. Manfredo Fanti, Balozi wa Umoja wa Ulaya;

Ndg. Mette Bech Pilgaard, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimaendeleo cha Ubalozi wa Denmark;

Ndg. Pamela O’Donnell, Balozi wa Kanada;

Ndg. Didier Chassot, Balozi wa Uswisi;

Ndg. Laurence Wilkes, Mkuu wa Utawala wa FCDO Ubalozi wa Uingereza;

Ndg. Lulu Ng’wanakilala, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF;

Wakurugenzi Mashirika, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi;

Wasaidizi wa Kisheria;

Wana habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana

Ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania………!

 

Awali ya yote, kabla sijaendelea na hotuba hii, ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa fadhila zake ambazo zimetuwezesha kukutana hapa leo kwa ajili ya kuadhimisha miaka kumi ya Taasisi ya Legal Services Facility(LSF) tukiwa na siha njema.

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana

Nimeanza kwa kusema tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa; pamoja na changamoto nyingi na hasa Ugonjwa wa UVIKO-19 ambao umeyumbisha dunia na kukatisha maisha ya wengi, sisi tumeendelea kuwa salama. Niwaombe wote tuendelee kumuunga Mkono Mama yetu Mh. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kuendelea kuchukua taadhari na pili kwa  sisi wenyewe kujitokeza na  kuhamasisha jamii yetu kupata chanjo ya UVIKO 19.

 

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Kipekee kabisa, napenda kuipongeza Taasisi hii ya Legal Services Facility kwa tukio hili muhimu la kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011. Tukio hili si tu muhimu kwa LSF, bali kwa nchi yetu hususani wadau wa ufikiaji na upatikanaji wa haki nchini kote.  Tukio hili ni nafasi ya kipekee kusherehekea mafanikio katika sekta ya ufikiaji na upatikanaji haki na pia kwa kiasi kikubwa linawezesha utambuzi wa maeneo ya ushirikiano na ufanyaji kazi pamoja baina ya Asasi za Kiraia zinazofanya kazi katika eneo hili, watendaji wa Serikali na sekta binafsi. Muitikio wa wadau mliohudhuria tukio hili, unaonesha dhahiri kuwa taasisi hii ni mshirika muhimu wa maendeleo na hushirikiana vyema na wadau wengine katika kuwahudumia na kuwafikia wananchi.

 

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Naipongeza pia Taasisi hii ya LSF kwa kuzindua mpango mkakati wake mpya wa Miaka mitano ijayo (2022-2026) mnamo mwezi Agosti mwaka huu, mpango ambao pamoja na mambo mengine, umelenga kufanya kazi kwa karibu na serikali na taasisi mbalimbali katika kuboresha sera, sheria na kuweka mazingira bora na wezeshi kwa jamii hususani Wanawake kwa kuainisha vipaumbele vitakavyoweza kusaidia upatikanaji wa haki nchini na kuchangia katika shughuli za uchumi na kuboresha maisha yao na familia zao kwa ujumla.

 

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana

Serikali yetu kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inatambua mchango wa Taasisi ya LSF katika kuwezesha ufikiaji wa haki nchini hususani kupitia huduma ya msaada wa Kisheria. Mchango wa Taasisi hii umekuwa ni wa muhimu sana hasa katika utungwaji na utekelezaji wa sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ambayo imeanzisha mfumo wa kisheria wa kutoa, kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa mashauri ya jinai na madai kwa watu wasiyo na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria kwa malipo kupitia wasaidizi wa kisheria (paralegals) ambao hadi sasa idadi yao ni zaidi ya elfu nne nchi nzima.

 

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Ifahamike kuwa, awali Serikali ilikuwa ikitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watuhumiwa wanaoshtakiwa kwa makosa makubwa tu kama vile mauaji, kuua bila kukusudia na uhaini. Huduma hiyo kwa muda mrefu ilikuwa ikitolewa na Mahakama Kuu pekee. Asasi mbalimbali za kiraia zilikuwa zikitoa baadhi ya huduma za kisheria kuanzia ushauri wa kisheria na uwakilishi mahakamani. Kazi hii ilikuwa ikifanywa pasipokuwa na uratibu baina ya taasisi hizo na Serikali. Utaratibu uliokuwa ukitumiwa na asasi za kiraia kwa kiasi kikubwa ulitegemea wafadhili ambao si wa kudumu na wenye matokeo ya muda mfupi.

Hivyo, kutokana na ongezeko la mahitaji, idadi ya watoa huduma ya msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria serikali ililazimika kuanzisha mfumo huu ili kuboresha huduma hiyo kuwasimamia na kuwaratibu. Kwa mantiki hiyo, Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 ililenga kuweka mfumo madhubuti na endelevu ambao utaziba ombwe lililokuwepo na kutoa suluhisho la changamoto zilizopo na kuhakikisha kuwa huduma ya msaada wa kisheria nchini inaleta matokeo chanya kwa ustawi wa wananchi, hususani, wa vijijini na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili.

 

Wageni Waalikwa

Mabibi na Mabwana

Pamoja na sheria ya msaada wa kisheria ya mwaka 2017, suala la upatikanaji wa haki linahusisha masuala kadha wa kadha katika jamii yetu, mojawapo ikiwa ni lugha inayotumika katika taasisi za upatikanaji wa haki nchini. Serikali katika kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki zinazotokana na matumizi ya lugha ya kiingereza katika Mahakama na Sheria zetu, kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali (The written Laws (Miscellaneous Amendments) Act No. 1 of 2020).  Pamoja na mambo mengine sheria hii imeitambua rasmi lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya sheria nchini Tanzania na kuelekeza sheria zote kutafsiriwa katika lugha ya kiswahili. Kipekee nipende kutambua mchango wa taasisi hii ya LSF kwa kutoa ushirikiano kwa Serikali kupitia wizara ya Sheria na katiba katika kuhakikisha sheria zinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na zoezi hili ambalo bado linaendelea kwa sasa linafanikiwa kwa ufanisi mkubwa.

 

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Serikali yetu pia kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW), inatambua mchango wa taasisi hii ya LSF hususani katika kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA 2017/18 – 2012/22) ambao uliandaliwa kwa kuzingatia Mipango na Mikataba ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kuhusu haki na ustawi wa wanawake na watoto.  Mipango na Mikataba hiyo ni pamoja na: Mkataba wa Kimataifa  wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (1979); Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989); Malengo ya Maendeleo Endelevu (2015); Ajenda ya Maendeleo ya Afrika Tuitakayo (2063); Mkataba wa Afrika  wa Haki na Ustawi wa Mtoto (1989); Sera ya Maendeleo ya Jinsia (2000); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Dira ya Maendeleo ya Taifa  (2025); Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka Mitano II (2016/17 – 2020/21) ambao kwa sasa tuko katika awamu ya tatu(2021-2026).

Lengo kuu la MTAKUWA ni kupunguza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/22. Katika kufikia lengo hili, Mpango kazi umebainisha afua mbalimbali za kimkakati zinazotekelezwa kupitia maeneo mahususi 8 ya utekelezaji ambayo ni: Kuimarisha Uchumi wa Kaya; Mila na Desturi; Mazingira Salama Sehemu za Umma; Malezi, Kuimarisha Familia na Mahusiano; Utekelezaji na Usimamizi wa Sheria; Huduma na Msaada kwa Waathirika wa Vitendo vya Ukatili; Mazingira Salama Shuleni na Stadi za Maisha; na Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini.

Serikali pia inatambua jitihada za kupinga ukatili wa kijinsia zinazofanya na Shirika la LSF Kuboresha madawati ya kijinsia yanayosimamiwa na wizara ya mambo ya ndani kupitia Jeshi la polisi nchini. Ningependa pia kuwapongeza kwa kuiunga mkono Serikali kufanya maboresho ya kiutendaji kwa jeshi letu la polisi kwa kuliwezesha kufanya mapitio ya kanuni za kiuongozi na majukumu ya jeshi hilo yaani Police General Orders (PGO).

 

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Ningetamani sana kuzungumza kwa hotuba ndefu sana jioni hii ya leo ila naomba nitumie msemo wa wahenga kuwa Wakati, ukuta. Napoelekea kuhitimisha hotuba yangu, nimalizie kusema kuwa kutokana na uzito wa shughuli hii sina budi kuwapongeza tena kwa kuadhimisha miaka 10 ya kazi ya upatikanaji wa haki nchini kupitia huduma ya msaada wa kisheria. Sisi kama serikali tunapenda kuwahakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi katika kazi na jitihada zote hususani katika utekelezaji wa mpango mkakati wenu mpya wa miaka mitano ijayo (2022-2026) ambao nimefurahi sana kusikia imezingatia mipango na vipaumbele vya serikali vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambao unaelezea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

 

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Mwisho kabisa, nitumie fursa hii kuziagiza taasisi za Serikali hususani zinazoshughulika na masuala ya upatikanaji wa haki  kufanya kazi kwa pamoja na Serikali pamoja na wadau wake kama LSF  katika kutoa huduma kwa wananchi lakin pia kufanya tafiti katika maswala ya upatikanaji haki nchini  na mchango wa hii sekta katika maendeleo ya nchi. Hii itasaidia katika kutoa huduma bora, endelevu na zinazokidhi mahitaji ya sasa. Niwaombe na kuwakaribisha pia na wadau wetu wa maendeleo kuendeleza ushirikiano wao kwa taasisi hii ya LSF na nyingine Nyingi  kwa maslahi mapana ya jamii yetu.

Nimalizie kwa kukushukuruni tena nyote na niwatakie maadhimisho mema ya Miaka kumi ya LSF.

Hongereni sana!

Mungu Ibariki Tanzania

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Author: admin

Leave a Reply

11 − 10 =