• admin
  • News & Updates
  • No Comments

LSF YAZINDUA HAKI YANGU APP, WANANCHI KUPATA MSAADA WA KISHERIA KUPITIA SIMU

Jumanne, Juni 15, 2021.  Dar es Salaam

Shirika linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania kupitia uwezeshaji wa kisheria, Legal Services Facility (LSF) leo Juni 15, 2021 limezindua mfumo wa kitumizi cha simu za mkononi (Mobile Application System) unaojulikana kama HAKI YANGU App, ambao, unaweza kumsaidia mwananchi kupata msaada wa kisheria popote alipo kupitia simu yake ya mkononi.

HAKI YANGU App ni mfumo uliobuniwa na LSF, ambao umewaunganisha wasaidizi wa kisheria takribani 4,000 nchi nzima, ambapo kupitia mfumo huo wanaweza kukutanishwa na mwananchi mwenye uhitaji wa huduma za msaada wa kisheria ama wasaidizi wa kisheria, na kuweza kumsaidia.

Mfumo huo ni wa kwanza kubuniwa na wa aina yake nchini Tanzania, ambao utamsaidia mwananchi kuwasiliana moja kwa moja na msaidizi wa kisheria au mtoa huduma za msaada wa kisheria kupitia simu ya mkononi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au kupiga simu.

Aidha, mfumo huo unaweza kumsaidia mwananchi kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria kwa kujifunza kupitia taarifa za jumla za masuala ya kisheria zilizowekwa katika mfumo huo kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya masuala yanayohitaji utatuzi wa kisheria kupitia mifumo rasmi na isiyo rasmi ya utoaji haki kama vile huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria. Halikadhalika mfumu huu utawezesha wasaidizi wa kisheria kupata mafunzo ya kozi mbalimbali kimtandao na kuendelea kuboresha uwezo wao ili kutoa huduma bora na yenye ufanisi zaidi

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kuwa, LSF imekuwa ni mdau muhimu wa serikali hasa katika sekta ya msaada wa kisheria kwakuwa imekuwa mstari wa mbele kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia mradi wake wa upatikanaji wa haki.

“LSF imekuwa ikichagiza mabadiliko ya kisera na kimfumo katika sekta ya msaada wa kisheria kwa kushirikana kwa karibu sana na serikali.  Mwaka 2017 tulishirikiana kwa karibu katika kuhakikisha sheria ya msaada wa kisheria inatungwa ili kuwezesha wananchi wetu kupata haki zao kupitia huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria;

“Pia, leo nimefurahi kuona LSF wamekuja na mfumo ambao utasogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi wanaohitaji huduma ya msaada na wasaidizi wa kisheria,” amesema Profesa Kabudi.

Profesa Kabudi ameongeza zaidi kuwa, serikali ya awamu sita inatambua mchango walionao wadau wa maendeleo nchini Tanzania ikiwemo sekta binafsi pamoja sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuunga juhudi za serikali kwenye kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma ya msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa ujumla kwani ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na uchumi kwa ujumla.

Serikali sasa iko katika kutekeleza mchakato wa kutafisiri sheria kwa  lugha ya Kiswahili hii ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha tunawawezesha wananchi kuelewa sheria na kudai haki zao pale zinapopotea

“Naipongeza sana LSF kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika hili la kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili  na kwa  kuendelea kutekeleza mradi wake mkubwa nchini Tanzania, ambao kwa kiasi kikubwa umeweza kusaidia maelfu wanawake na watoto kupata haki zao kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima.  Naamini kupitia mfumo huu pia, wananchi wengi hususani kina mama na watoto wataweza kupata msaada wa haraka zaidi pale wanapokutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuminywa ama kukandamizwa kwa haki zao kutokana na sababu kadha wa kadha kama vile jinsia au umri wao,” ameeleza Profesa Kabudi.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa, LSF imebuni mfumo wa HAKI YANGU App ili kuendelea kuhakikisha kuwa, huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini Tanzania zinapatikana kiurahisi zaidi kwakuwa upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa ni changamoto kupatikana katika jamii licha ya umuhimu wake.

“Kwa uzoefu wa LSF katika kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini tumeona kuwa, wananchi walio wengi bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto hivyo njia hii itachochea  upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi zaidi mahali popote kupitia simu ya mkononi .

“Kwa miaka 10 sasa, sisi kama LSF tumekuwa tukiwezesha mashirika yanayotoa huduma za msaada na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 200 nchi nzima ili kutoa huduma hiyo muhimu katika jamii bure.  HAKI YANGU App ni muendelezo tu wa utekelezaji wa mradi wetu unaolenga kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria bure kwa wananchi wote.” Amesema Mtendaji huyo mkuu wa LSF.

LSF ni Shirika linalofadhiliwa na wadau wa maendeleo, ambao ni Umoja wa Nchi za Ulaya nchini Tanzania na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kupitia ubalozi wa Denmark chini katika kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini Tanzania.

Chini ya ufadhili huu LSF inatekeleza mradi wa upatikanaji wa haki katika kila mkoa na wilaya Tanzania bara na Zanzibar ambapo takribani watu millioni 6 wanafikiwa kwa kupatia elimu juu ya maswala ya kisheria  na  kesi takribani 90,000 zimewafikia watoa huduma za msaada wa kisheria ambapo asilimia 60% za mashauri hayo yameweza kutatuliwa na watoa huduma hao. (repoti ya LSF 2020) Hii kwa kiasi kikubwa imepunguza msongamano wa kesi katika mahakama na kupunguza gharama ambazo zingetokana na kusimamia na kuendesha kesi hizi

Kuwepo kwa App hii kunaenda sambamba na kukua kwa technologia na hivyo kutatchochea upatikanaji wa haki kwa makundi mbalimbali kwa wakati mahali na wakati wowote.

 

 

 

 

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2020 LSF ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 10.4 za kitanzania kwa ajili ya kuyawezesha mashirika zaidi ya 2020 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria nchini.

MWISHO=======

Kwa mawasiliano zaidi tembelea tovuti yetu www.lsftz.org au wasiliana na;

 

Jane Matinde – Meneja Mawasiliano – LSF

Email: jane.matinde@lsftz.org

Mobile: +255784 670 232

 

AU

 

Mtapa Kitwaza – Afisa Mawasiliano – LSF

Email: mtapa.kitwaza@lsftz.org

Mobile:  +255684 738 499

Author: admin

Leave a Reply

eleven − ten =